Tuesday, September 30, 2014

UCHUMBA SI MAZOEA



SOMO: MAZOEA SI UCHUMBA

WALIMU: NANGI & STEPHEN WEREMA
1.     MAZOEA NI NINI?
MAZOEA ni ukaribu kati ya Mtu na Mtu.  Kwa asili ya mwili, mtu anavutwa kujenga mazoea na jinsia tofauti na kwetu vijana hii ni changamoto.

2.     MAMBO YANAYOLETA MAZOEA AU YANAYOONESHA MAZOEA  NI:
a.      Mazungumzo                  -           Mazungumzo ya mara kwa mara
mdomo kwa mdomo au kwa simu.
b.     Ziara za pamoja             -           Kutembeleana mara kwa mara
Kutembea pamoja mara kwa mara.i
c.      Kumjali/kujitoa zaidi            -           Kumjali/kujitoa zaidi kwa  mtu mmoja
Kuguswa zaidi na mambo yake yeye tu.    
d.     Zawadi/offer kwake   -           Zawadi hupelekea mazoea au hutolewa
baada ya kuwepo na mazoea ya watu hao.
Haya ni baadhi tu ya maeneo yanaoonesha mazoea baina ya mtu na mtu au yanakuwa sababu ya watu hawa kuzoeana kupitia mambo hayo hapo juu.

3.     BAADHI YA MAENEO MUHIM KUWEKA MIPAKA ILI KUEPUKA MAZOEA
Mazoea si jambo zuri kulikumbatia maana linaua kwa kasi MIPAKA yetu.  Andiko la 1Petro 2:16 inafafanua vizuri kuhusu uhuru wetu sisi tuliookoka.
Pamoja na uhuru huo ni muhumu kujua pia tu watumwa wa Bwana.  Hivyo ni vema kuzingatia kuwa UHURU wetu una MIPAKA kwa kila eneo siku zote.
a)    Mazungumzo-Tuko huru lakini tuna MIPAKA katika KUZUNGUMZA.
Nazungumza nini? Nazungumza na nani? Nazungumza wapi? Je, haya yanampendeza Bwana wangu Yesu maana mimi ni Mtumwa wake.
Kijana asiye na Ndoa haruhusiw kuzungumza mambo ya Ndoa na mtu.
Aliye katika Ndoa pia haruhusiwi kuzungumza ndoa na asiye mwenzi.
b)    Ziara-Tuko huru lakini tuna MIPAKA katika kutembelea/kuambatana.
Ni aibu kijana ulieokoka ziara zako kaka ni kwa wadada, dada kwa kaka.
c)     Mawasiliano-tuko huru lakini tuna MIPAKA katika Mawasiliano yetu.
Na hili linajumuisha mipaka katika muda, ishara, lugha na vitendo katika mawasiliano.   Usiwe kaka/dada kata wewe, kata wewe ni hatari, epuka.
d)   Kusaidiana-tuko huru lakini tuna MIPAKA katika masaidiano yetu pia.
e)    Upendano-tuko huru lakini tuna MIPAKA katika Upendano-Ebran 13:1.
Ni kweli Biblia inatuagiza upendano wa ndugu na udumu. Tunadumisha huku tukizingatia MIPAKA hasa kwa vile kuna mvutano wa kimaumbile.
Biblia inaagiza katika kila eneo tujipatie sifa njema – 2Kor 6:3-10 [3-4].
4.     BAADHI YA MAMBO YANAYOTOKANA NA MAZOEA, YANAVYOUMIZA:

(1)            Tabia ya Mtu mwenyewe Mvulana au Msichana hamaanishi katika maamuzi yake. Anamzoea mtu sana mwisho anaahidi uchumba au anachomekea maneno ya mvuto, “unavyompenda Mungu, sijui nani huyo atakayebahatika kukuoa/kuolewa na wewe”. “Nikibahatika mimi mbona nitatoa sadaka ya shukrani”. Mtu anajipa moyo labda haya maono yangu, anapojaribu kujiachia aiingie nafasi, mwenzie anaanza kuweka mipaka sasa kwa nguvu zote-inaumiza.

(2)            Ukaribu kati ya Vijana [Kike/Kiume] unapodhaniwa ni uchumba.
Yamkini wote wawili au mmoja wapo amejihesabia ni mchumba.  Sasa akitokea mchumba halisi ndio maumivu kwa aliyedhania ndiye.
Ndipo unakuta uchumba unatangazwa mtu huku kilio-inaumiza.

(3)            Kutoa au Kupokea zawadi huleta mazoea na kumuumiza mmoja.
Aliyezoea kupokea vitu/offer siku akikatizwa asipewe ni maumivu.
Kadri unavyotoa au kupokea zawadi inaleta dhana ya uchumba.
Anayetoa zawadi anaona kwa zawadi hizi nadhan amenielewa.
Anayepokea anasema moyoni kwa zawadi hizi mimi ni mchumba tu.
Ikitokea ameambulia zawadi tu lakini mtu amemkosa ni maumivu.

(4)            Kupenda kutembea, kukaa au kusimama[minazi] pamoja kama kumbikumbi huletwa na mazoea. Ukimuona dada huyu lazima utamkuta na kaka fulani. Bila kujua wapo Kanisani lakini wanautii mwili badala ya kuutiisha maana kwa asili ya mwili kila mmoja huvutwa kwa mwenzie.  Ila ukimaanisha katika wokovu asili ya mwili inafishwa asili ya roho ambayo iko radhi kufanya mapenzi ya Mungu inahuishwa.  Hali hii inapoendelea sana mtu haendi semina mpaka ampitie huyu, kwenye matamasha amekaa nae, wakitoka Kanisani wako wote na wanakunywa soda wote yeyote anatoa offer.
Mwisho wote wawili au mmoja wao moyoni anajidhania ni uchumba huu. Hatari zaidi wengine wanawadhania ni wachumba. U-dot com huu, unaziba mlango hasa kwa binti kuchumbiwa. Kwa dhana kuwa ni mchumba wa mtu, kumbe huyo anaye dhaniwa naye hanampango wowote na bint ni mazoea tu na kuvutwa na mwili anajkuta muda wote yuko chini ya kwapa za bint akiuliza anaruka.
>Mchumba halisi anashindwa kutangaza nia akijua ni dada wa mtu.  >Hata akijitosa rasmi dada anakataa akimngoja huyo aliyemzoea. >Huyo anayedhaniwa na watu au na binti husika kuwa ni mchumba                   wa mtu anapotangaza nia na dada mwingine ndio maumivu hayo.
 >Kimsingi si mchumba hajatamka lolote, hajachukua hatua yoyote ila dada au kaka husika utashangaa anaanza kummiliki kama wake. >>Akiongea na mtu Kanisani ananuna au anauliza mlikuwa mnacheka nini pale, ana wivu kweli maana anataka awe nayeye tu.
>>Dada/Kaka akiona wivu huo anajipa moyo kumbe wa mazoea tu.
>Kulichafua Kanisa na kuharibu ushuhuda kwa mazoea hayo ya masaa 24 kaka/dada yuko chini ya kwapa za mwenzie watu hawatuelewi wala hatuna lugha ya kuwaambia wakaelewa hata kama vijana hawafanyi dhambi kwa hilo tu wanazuilia watu mbingu.
           
(5)            Kuvuka mipaka katika kuhudumiana/kusaidiana kama dada/kaka.
Mazoea yakilelewa na vijana mwisho huleta tatizo la kusaidiana au kuhudumiana kuliko vuka mipaka yetu kama vijana tuliookoka. Inafikia hatua eti kaka anaumwa anamwita dada aje amfulie nguo.  Au dada anaumwa anamwita kaka aje kumfulia nguo. Wanapikiana hadi chakula mgonjwa, anazidiwa eti kaka analishwa uji na dada au dada analishwa uji na kaka. Huyo mgonjwa si ataumwa kila siku apate ‘offer’ hiyo ya kulishwa na huyu anafurahia ‘tender’ ya kulisha. Kodi ya nyumba, matatizo ya familia [ugonjwa/msiba] vyote anaanza kuhudumia huyu dada/kaka wa mazoea, pengine kwa kuomba asaidie chochote au kwa uso kuumbwa na haya ameshirikishwa tatizo la familia inabidi aoneshe ushiriki wake. >Ikitokea dada/kaka wa jinsi hii amefanya maamuzi ya kukata huduma au kukataa kuhudumiwa nae ili afanye maamuzi-inaumiza.
>Ikitokea kaka/dada amepata mchumba hasa kwa vile anaona huyu hatangazi nia anapokea au anatoa huduma tu, huyu wa mazoeani aliyekuwa anafua, kupika na kuhudumia anaumizwa na hilo.

(6)            Mazoea huchochea mapenzi kabla ya wakati wake-Wimbo bora 3:5
Biblia inaonya kwa ukali tu kuwa vijana tusiyachochee mapenzi.  Mazoea yanapolelewa huuwa mipaka yote ya kaka na dada katika Bwana. Wanahudumiana/kusaidiana bila tahadhari [kulishana], wanaambatana kila mahali na wakati wote ni kosa la jinai, mwisho wanawaka tamaa hapo wanajikuta kutoka mazoea hadi kitandani.
Wamewakatamaa-wasipofanya wanaumiza miili yao iliyochochewa.
Wamewakatamaa-wakifanya wanaumiza roho na kuangamiza nafsi.
Ni heri kuyaepuka mazoea kuliko kuingia katika mtihani huu.

(7)            Mazoea huleta maumivu hadi ndani ya Ndoa maana husababisha mtu kuoa/kuolewa na asiye wake, ni maumivu.  Jamani mke mwema/mume mwema hapatikani katika mazoea Biblia inasema mke mwema mtu hupewa na Bwana-Mithali 19:14 si na mazoea hili limeumiza wengi waliopewa ndoa na mazoea.  Mimi na Steve mpaka anakuja kuniposa hatukuwa na mazoea.  Mungu hasaidiwi kazi kwa mazoea, lililo la Mungu litasimama tu.

Kwa jinsi gani mazoea hupelekea mtu kuoa/kuolewa na asiye wake?
a.      Mazoea hufanya mtu akose msimamo katika kufanya maamuzi.
·     Hata kama anajua huyo wa mazoea siye anakosa ujasiri wa kumkataa kwa jinsi walivyozoeana [waswahili wanasema uso umeumbwa na haya].  Anaamua kumkubali wala hata haombi.
·     Moyoni anamsikia mtu mwingine mazoea yanampa mtu mwingine. Mwisho anakosa msimamo anampokea mtu siye.

b.     Mazoea huleta moyoni mguso feki si mguso halisi wa Ki-Mungu.
·     Moyoni huwa na mguso halisi wa Ki-Mungu kwa aliye wako.  Mguso huo ndio utadumu nao maisha yako yote ya ndoa.  Hata kama Nangi aliyenioa nimekuwa na muonekano tofauti bado mguso huu utakuwepo kama siku ya kwanza aliponiaona na mimi vivyo hivyo. Kukosa Mguso huu ni maumivu ktk Ndoa.
·     Mazoea nayo huleta mguso wake moyoni kwa ukaribu wenu.
Mguso wa mazoea ni wa msisimko tu wa mwili na Mguso huu unatokana na muonekano wa nje, mguso huja na kuondoka.
Mfano: Mguso umetokana na wembamba wa binti akimuoa akanenepa kila siku atasimangiwa huo unene, “punguza kula bwana umefutuka utadhani kifutu”, wembamba umeondoka na mguso umeondoka, kaka ametoka mtambi huo, “huo mtambi wako unazidi tu sijui utafika wapi fanya zoezi uko” mwili wa kati umeondoka na mguso unaondoka. Mguso huu ni wa ukaribu tu ukiondoka na mguso unaondoka-[fimbo ya mbali haiui nyoka], ukihama hapo mara hata ndoa usiifikie. 
·     Mungu huleta mguso wake moyoni ili kuifanya ‘right couple’.
Mguso huu wa Ki-Mungu humpenda mtu bila sababu yoyote.  Yamkin ni kaka nadhifu/mtanashati kwel ila mguso zaidi ndan
Dada mrembo no.8, sauti ya filimbi ila mguso wako ni ndani.
Hata hayo yasipokuwepo mguso wako utakuwepo hapo tu.
Miaka ikiendelea kidogo tu kama sisi ni miaka 12 ya ndoa yetu kuna mabadiliko tabia ya mwili yanaibuka hayakwepeki kwa kaka na dada wote tumebadilika bado mguso huu haubadiliki. Tafuta mguso wa Ki-Mungu moyoni si wa mazoea-utaumia
c.      Mazoea huleta deni kwa mliyezoeana na kuwiwa kulipa fadhila.
Anakutaka uchumba ili tu kulipa fadhila hizo za kum-company.
Anakukubali wewe si kwa kumtii Mungu bali ili kulipa fadhila.

d.     Mazoea huleta Makwazo yasiyo ya lazima kabla/baada ya ndoa.
·          Endapo mtu atamchumbia mtu mwingine ni makwazo.
·          Endapo mtu atatangaza nia na kukataliwa ni makwazo.
·        Ndani ya Ndoa atakwazika ovyo, unene unamkwaza, kitambi kinamkwaza, uso aliovutiwa sio huo tena nao unamkwaza, shape na.8 imebadilika imekuwa 9 inamkwaza,n.k. inaumiza.

e.      Mazoea huleta Ndoto zenye dhana ya uchumba kumbe si kweli.
Ndoto usingizini unaota unamuoa/unaolewa na huyo kabisa unajifariji ni Mungu anakuonesha mwenzi wak kumbe ni mazoea yanaokuonesha. Watu mko pamoja masaa 24 chini ya kwapa usimuote jamani?  Utamuota hata mko ‘honeymoon’ kabisaa.

f.       Mazoea hutumika kama njia ya kumpata mchumba kwa hila.
Biblia inasema mambo yote yatendeke kwa utaratibu-1Kor 14:40
Mazoea hayalijui andiko hili yanavunja utaratibu yanatumika kama nguvu ya ushawishi [convincing power] ili achumbie/we.  Mtu anapodhani amepata kumbe amepatikana, anaoa/anaolewa na asiye wake kwa uzembe ama wa kuutii mwili, au kutojiamini na kutomuamini Mungu wake kuwa anaweza kumpa mke/mume mwema bila ya kutumia mazoea. Ndani ya Ndoa aliyenogewa na akashawishika analia nawewe shawishi utalia. Kuna watu wanaoana hata hawajui walichumbiana lini, wameanza mazoea wakaunga juu kwa juu, eneo nyeti kama ndoa, huombi? shetani anakupiga bao kiulaini wala si kiufundi-aibu hii kwa waaminio.

g.      Mazoea hutumika kama njia ya kumnasa mtu katika dhambi.
Mazoea haya yameangusha vijana wengi katika uasherati. Kadri wanavyozoeana wanaua MIPAKA yao polepole na mwili unataka. Wanajifanya vijana wa dot.com wamejikuta ni wa dot.koma. Maana wameswagwa na shetani mpaka wamekoma wenyewe.

5.     HITIMISHO
Mazoea ni silaha ya shetani kwa vijana kama uliyaanzisha yavunje haraka ili ujipange kiroho kumtafuta mwenzi si ki mazoea-utaumia. Mazoea yanagharama kubwa kuvunja kama hujaingia Usiyaanzishe.

No comments:

Post a Comment